
Kavumbagu ambaye mkataba wake uliisha msimu uliopita, alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Azam juzi kwa ajili ya kuwatumikia mabingwa hao msimu ujao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkwasa alisema Kavumbagu bado mchezaji mzuri anayemwamini, ndio maana walikuwa wakimtumia katika mechi nyingi msimu uliopita na bado walikuwa wakimhitaji.
“Ni mchezaji mzuri, alikuwa akifanya vizuri na bado tulikuwa tunamhitaji ndio maana tuliweza kumtumia msimu mzima wa Ligi Kuu Tanzania Bara, amefanya haraka mno,”alisema.
Mkwasa alisema walihitaji kuwa naye lakini kama mwenyewe ameshindwa kuvuta subira na kukimbilia Azam, basi, hawawezi kumlazimisha.
Alisema kwa utaratibu wa Yanga huwa mchezaji anapomaliza mkataba wake, humwita na kuzungumza kumpa mwingine, hivyo, kama angeendelea kusubiri angeitwa na kuongezewa mkataba mwingine.
Kavumbagu alimaliza msimu wa Ligi Kuu akiwa amepachika mabao 13, nyuma ya Mrundi mwenzake anayecheza Simba Amis Tambwe aliyeibuka mfungaji bora kwa kupachika mabao 19.